ABDULKARIM SUMA





Thursday, October 31, 2013

Taarifa kutoka Mahakamani kuhusu rufaa ya kifungo cha Babu Seya na Papi kocha maisha jela



Babu SeyaMahakama ya rufani Tanzania imeanza kusikiliza rufaa ya mwanamuziki maarufu Tanzania Nguza Viking (Babu Seya) na mwanae Johnson Nguza (Papii Kocha) ambao wanatumikia kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya ubakaji na ulawiti wa watoto.
Katika rufani hiyo iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufani ambao ni Mbarouk mbarouk, Salum Massati
na Nathalia Kimaro, wakili wa upande wa mashtaka Mabele Marando amesema amekata rufaa kutokana na kutosikilizwa kwa shahidi muhimu kwenye kesi hii ambae alitajwa kuwa ndie aliwapeleka watoto hao kwa babu Seya.
Marando amesema pia ushahidi wa kuunga mkono ushahidi uliotolewa na watoto haukuzingatia sheria baada ya mahakama kutembelea nyumbani kwa babu Seya na kumuhoji mtoto bila ya kiapo hivyo ameomba Mahakama ipitie upya hukumu hiyo ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
Baada ya kuwasilishwa kwa maombi hayo, wakili wa serikali Jackson Bulashi akiwa na wenzake wanne amepinga maombi yaliyotolewa na upande wa mlalamikiwa na kubainisha kwamba hoja zilizowasilishwa Mahakamani zilipaswa kuwasilishwa awali wakati kesi hiyo ilipokua inasikilizwa.
Wakili huyo wa serikali ameiomba Mahakama kutupilia mbali maombi hayo kutokana na kutoainisha athari za moja kwa moja kwa washitakiwa na kutaka adhabu ya kifungo cha maisha iliyotolewa dhidi ya babu Seya na Papi Kocha iendelee kutekelezwa.
Baada ya pande zote mbili kutoa maelezo yao mbele ya jopo la majaji watatu, Mwenyekiti wa jopo hilo Jaji Nathalia Kimaro ameahirisha kesi hii ili kutoa nafasi kwa majaji kupitia maelezo yote yaliyotolewa na kuyatolea maamuzi.
Mwaka 2004 Babu Seya na wanae watatu walihukumiwa kifungo cha maisha jela na hakimu mkazi Addy Lyamuya wa Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar es salaam ambapo baada ya hukumu hiyo, February 2010 walikata rufaa Mahakama kuu ya Tanzania ambayo iligonga mwamba mbele ya jaji Thomas Mihayo wa Mahakama hiyo.
Jopo la majaji lililosikiliza rufaa hiyo ndilo lililosikiliza awali na kuwaachia huru watoto wawili wa Babu Seya ambao ni Nguza Mbangu na Francis Nguza baada ya kuonekana hawakuwa na hatia.

0 comments:

Post a Comment