Wakazi wa jiji la Dar Es Salaam
wamejitokeza kuaga mwili wa mama mzazi wa mwandishi wa ITV Radio one
Ufoo Saro marehemu Anastazia Saro katika kanisa la kiinjili la kilutheri
Kibwegere Kibamba kabla ya kusafirishwa kwenda Moshi kwa mazishi.
Kutokana na msiba huo,ITV ilianza kwa kufika katika
hospitali ya taifa ya Muhimbili ili kumjulia hali mwandishi wa ITV
Ufoo Saro aliyelazwa katika hospitali hiyo ambapo afisa uhusiano wa
hospitali hiyo bwana Aminiel Aligaesha amesema anaendelea vizuri.
Baada ya afya ya Ufoo Saro inavyoendelea, ITV
ilitia kambi katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali hiyo na
kushuhudia mwili wa Anastazia Saro ukiondolewa na kupelekwa Kibamba
nyumbani kwake ambapo umati mkubwa wa watu walipokea mwili huo kisha
kuingizwa ndani huku vilio vikitawala.
Mwili ulifikishwa katika kanisa la KKKT Kibwegere
Kibamba na kupokelewa na umati mkubwa wa watu waliofika ndani ya kanisa
hilo,ambapo mchungaji wa kanisa hilo Magreth Chikolowa amesema kuwa kuna
vifo vingine vinatokea lakini si kwa kusudi la Mungu huku msemaji wa
familia akieleza historia fupi ya marehemu.
Mkurugenzi wa ITV Radio one Bi Joyce Mhaville kwa
niaba ya mwenyekiti wa makampuni ya IPP Dr Reginald Mengi amesema
wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mama yake Ufoo na kwamba
mbali na kuwepo hapo kwa ajili ya mwenyekiti wa makampuni ya IPP lakini
ameagizwa na Ufoo Saro kumwakilisha katika kumuaga mama yake huku
mwenyekiti wa kamati nzima wa msiba huo akitoa shukrani kwa mwenyekiti
wa makampuni ya IPP kwa kufanikisha safari ya kusafirisha mwili huo kama
anavyoeleza.
Ndugu jamaa na marafiki waliaga mwili huo kwa
majonzi huku baadhi ya wafiwa wengine wakishindwa na kupewa msaada wa
kushikwa huku vilio vikitawala ambapo marehemu Anastazia Saro ameacha
mtoto mmoja Ufoo Saro na mjukuu mmoja Alvin ambapo anatarajia kuzikwa
katika kijiji cha Shali Machame mkoani Kilimanjaro.
0 comments:
Post a Comment