ABDULKARIM SUMA





Wednesday, January 15, 2014

ANGALIA ALAMA HIZI, ANZA MWAKA NA FIKRA MPYA!-3


KAMA hutajitambua na kujithamini, hatatokea mtu wa kukujulisha kuwa wewe ni mwenye thamani. Maisha yako ni muhimu, afya yako pia ni muhimu sana. Kila kitu chako kina umuhimu wake, lakini usitegemee mtu akueleze, anza wewe!

Marafiki zangu tunaangalia namna ya kugundua penzi la kweli na kusimamia katika uhusiano ulio sahihi. Nilieleza katika matoleo yaliyopita kuwa, ni vizuri kuwa kwenye uhusiano wenye malengo.
Kwamba kudumu kwenye uchumba kwa muda mrefu siyo tiketi ya kuingia kwenye ndoa. Kama ndivyo ni vyema sasa kuangalia mahali ulipo ili uchukue hatua stahiki.
Nilianza kwa upande wa wanawake ambapo nilieleza sifa za wanaume ambazo zinamuweka katika nafasi ya mume wa baadaye. Leo sasa nageukia kwa wanaume kwa kuwaeleza baadhi ya alama za hatari walizonazo wanawake ambao hawana mipango nao ya baadaye.
Unaweza kuwa na mwanamke kwa muda mrefu, kumbe ana mambo yake, hana nia na wewe isipokuwa anakufanya kitega uchumi tu cha kumrahishia mambo yake.

Tuendelee kujifunza marafiki...
Usanii mwingi...
Mwanamke ambaye hana nia na wewe unaweza kumjua kwa kumtizama anavyokuwa na usanii hata katika kudeka kwake tu! Mwanamke ana haki ya kudeka kwa
mwanaume wake, lakini siyo kwa nia nyingine yoyote zaidi ya kunakshi penzi.
Huyu hana nia hiyo, anadeka kwa ajili ya kukupagawisha kimahaba ili akukoleze. Mchunguze vizuri, utagundua kwamba hata sauti yake anayoitumia kuzungumza na wewe
siyo anayotumia akiwa na shoga zake. Anailegeza na kuiremba kwa kila hali.
Anataka kukupagawisha. Hiyo ndiyo nia yake, kukupagawisha sana maana yake hutapindua na hutakuwa na wazo la kuwa na mtu mwingine zaidi yake. Kwani kwako amelenga nini zaidi ya fedha?

Mizinga mingi!
Ni kawaida mwanamke kumwomba pesa mpenzi wake, lakini huyu asiye na mapenzi ya kweli, huwaza pesa mara zote. Hata kama utazungumza kuhusu kutoka naye, bado

ataulizia kuhusu dau lake. Ana mahitaji mengi, mara rasta, nguo mpya zimeingia, vocha na hata mahitaji mengine ambayo kimsingi hayakuhusu sana.
Mbaya zaidi, hata kama utakuwa mgonjwa na amekuja kukutizama siyo ajabu akakuomba pesa. Fanya utafiti wako vizuri, vuta kumbukumbu uone kama ana tabia hii. Kama ndiyo, hakufai!
Heshima sifuri.
Kwa kuwa hakupendi na wala hafikirii kuwa na wewe katika ndoa, sifa za uanamke hatakuwa nazo. Inawezekana kabisa anazifahamu vizuri sana sifa hizo lakini hana muda.
Hasikii ukimwambia kitu, mjeuri na wala haheshimu kauli zako. Kama mpenzi wako, ambaye una malengo naye ya baadaye, una haki ya kumzuia aina fulani ya mavazi, kampani au tabia ambazo huzipendi... kwa mwanamke wa aina hii, kumwambia ni sawa umemruhusu!

Mtundu balaa!
Utundu faragha unakubalika kunakshi penzi, lakini kwa mwanamke ambaye amekufanya kitega uchumi ni mkali zaidi upande huu. Anaweza akakosa sifa zote, lakini akawa

anakupeleka puta kwenye sita kwa sita! Anafanya haya kwa sababu ndiyo silaha yake ya mwisho.
Hata hivyo siyo kila mwanamke mwenye uwezo mkubwa faragha anaweza kuwa tapeli wa mapenzi, lakini wengi wao huwa wanawapagawisha wapenzi wao ili wakitaka

Kuwaza kuwaacha, wahofie kukosa mapenzi. Hili nalo ni la kuchunguza.
 
Msiri kupitiliza
Ni mpenzi wako, lakini ni msiri kuliko kawaida, ni msiri wa mambo yake, lakini pia hataki uhusiano wenu ujulikane. Hata kama utamwambia unataka kujulikana na ndugu

zake, hatakubali. Anasingizia bado ni mapema sana wewe kwenda kwao.
Ni lini mwanamke akakataa mwanaume mwenye msimamo asijitambulishe kwao? Hata kama unampenda sana, lakini unapoona alama hii lazima uwe makini.
Huenda alishapeleka msururu wa wanaume au tayari yupo au hakupendi tu! Kwa maneno mengine, amepoteza sifa ya kuwa mke wako.

Hukushusha kiaina
Hapa mwanamke wa aina hii hashindwi kukuonesha dalili kwamba wewe siyo chaguo lake. Mwanamke huyu ni mjanja sana na mwenye akili nyingi kweli kweli.
Anapanga mipango yake taratibu, anaifanyia mazoezi kabla ya kuonesha wazi. Hapa atakuonesha kwamba huna sifa, anaweza akamuona mwanaume fulani kwenye filamu,

gazeti au jarida akamsifia sana.
Hata kama mmetoka naye, anaweza kumsifia mwanaume mwingine aliyepita karibu yenu. Kifupi anaonesha kwamba wewe huna sifa ya kuwa naye. Anakushusha thamani yako waziwazi.
Kama mwanamke anaonesha wazi kuwa huna sifa, una sababu gani ya kuwa naye? Una sababu gani ya kumfikiria kuwa anaweza kuwa mkeo?
Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

0 comments:

Post a Comment