ABDULKARIM SUMA





Wednesday, January 15, 2014

TAFF, BONGO MUVI, NANI ALIYEWAROGA?

KWENU,
Uongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) na Klabu ya Bongo Movie Unity ‘Bongo Muvi’. Bila shaka ni wazima na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku salama kabisa.

Kuna jambo nahitaji kuwashauri maana naona kama msipoliweka sawa, hali inaweza kuwa mbaya na mkaibomoa sanaa yenu kwa mikono yenu wenyewe. Kuna kipindi fulani huko nyuma niliwahi kusikia mgogoro wa chinichini kati yenu.
Hoja hasa za tofauti hizo naweza kusema zilikuwa zinazungumzika vizuri tu, lakini mkakuza na kufanya hali ya kisanaa iwe mbaya kwa upande wenu. Inawezekana msione tatizo kwa sasa lakini siku zijazo mtakuja kugundua, muda ukiwa umeshawaacha!
Hivi karibuni, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ aliibuka kidedea katika uchaguzi wa klabu yao ya Bongo Muvi ambapo aliibuka kuwa mwenyekiti mpya akiwa na viongozi wengine. Aliahidi mengi. Nilipata kuzungumza na Steve na kumwuliza mambo kadhaa kuhuasiana na mikakati yake katika uongozi wake mpya.
Alieleza mengi lakini kubwa alisema atashughulikia tatizo la maadili ambalo alikiri lipo kwenye klabu yao lakini pia alisema atahakikisha sanaa inapata heshima na masilahi ya wasanii yanaboreshwa.
Cha ajabu sasa, wikiendi iliyopita nimesoma katika gazeti moja linalotoka kila siku, Mwenyekiti wa TAFF, Simon Mwakifwamba, alipoulizwa kuhusu Bongo Muvi hasa wanasimama chini ya mwavuli gani, alisema TAFF hawaitambui!
Hapo sasa ndipo nilipopata shaka. Kama mwenyekiti wa shirikisho haitambui Klabu ya Bongo Muvi, mwenyekiti wake, Steve Nyerere atafanyaje kazi? Atawezeje kushughulikia kero za wasanii?
Ilivyo ni kwamba, TAFF ndiyo mama wa vyama vyote vya sanaa ya maigizo nchini. Mfano, kuna Chama cha Waigizaji, Chama cha Waandishi wa Miongozo ya Sinema, Chama cha Waongozaji nk. Bila shaka, hata Bongo Muvi inapaswa kuwa chini ya TAFF.
Hapo kuna tatizo gani? TAFF na Bongo Muvi kuna uhasama gani? Kwa nini msikae chini na kuangalia namna ya kuondoa hizo tofauti zenu mkafanya kazi? Naanza kuingiwa na wasiwasi kwamba, si ajabu matatizo yaliyopo yanaweza kuwa binafsi – kati ya mtu na mtu.
Kama sivyo, basi mnatakiwa kujua kuwa, mpo kwa ajili ya wasanii na sanaa ya Tanzania kwa ujumla wake. Acheni ubabaishaji na malumbano ya kwenye magazeti ambayo hayana maana.
Tumeona mifano mingi katika vyama tofautitofauti vya sanaa au michezo. Mnapoingiza malumbano ni rahisi kuharibu kila kitu. Lazima dawa ya kudumu ipatikane.
Hamtaweza kujenga sanaa kwa ugomvi, chuki, ubabe au kila mmoja kutaka kuonekana yeye ni zaidi. Heshima ni kitu cha msingi zaidi. Busara ikitumika hakuna kitakachoharibika.
Nahisi kuna dalili za kuogopana kati yenu; inawezekana TAFF ina hofu na Bongo Muvi kwa sababu ina mastaa wengi, si ajabu Bongo Muvi nao wanajisikia na wanajiona wapo juu ndiyo maana hawaoni sababu ya kumaliza tofauti zao.
Vyovyote iwavyo, lazima mkubali kuweka tofauti hizo pembeni kisha mkutane kwenye meza moja ya mazungumzo muweke mambo sawa. Inawezekana mkitaka, lakini kama lengo lenu ni kuua sanaa ya maigizo, endeleeni na bifu lenu.

0 comments:

Post a Comment